Kamati ya waamuzi nchini inatarajia kuanza kuwanoa marefa 100 watakaotumika kwenye michezo ya Ligi Kuu inayoanza juma lijalo pamoja na Ligi ya Championship itakayoanza mwezi ujao.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nassoro Hamduni amesema tayari wamekamilisha zoezi kwa waamuzi wenye kitambaa cha FIFA, zoezi ambalo lilianza tangu Agosti Mosi na kufungwa juzi Jumamosi (Agosti 05).
Hamduni amesema katika semina hiyo waamuzi walikuwa 34 na Bara walikuwa 28 na sita kutoka visiwani Zanzibar na kati yao wanne walipata tatizo la kiafya katika mtihani wa utimamu wa mwili (kukimbia).
“Sio vyema kuwataja majina sababu bado wataendelea kutambulika kama waamuzi wenye beji ya FIFA na wanayo nafasi ya kujirekebisha sababu zoezi hili linadumu mwaka mmoja,” amesema Hamduni na kuongeza;
“Tutaangalia wapi FIFA wanafanya zoezi hili baada ya hapa, hivyo nao watakwenda huko lakini kwa sasa haiwaondolei sifa ya marefa wa FIFA hapa nchini, hivyo wakifanya vyema kwenye michezo au wakaenda sehemu nyingine kukimbia na kufaulu itakuwa vyema.”
Licha ya Hamduni kutotaja majina yao lakini imefahamika waamuzi hawa ni Jonesia Rukyaa, Hance Mabena, Ester Adalbert wote wanachezesha na Soud Lila mwamuzi wa pembeni.
Pia Hamduni aliongeza leo linaanza zoezi kwa waamuzi watakaopangwa kuchezesha Ligi Kuu na Ligi ya Championship nao wataanza semina na mafunzo hadi Agosti 13 na kisha kupangiwa ratiba.
“Mwaka huu hatujajua hadi sasa idadi kamili ya waamuzi tutakaokuwa nao kwenye Ligi Kuu na Ligi nyingine hadi pale tutakapopewa maelekezo na TFF ndio maana tumeita waamuzi wengi (100) tukijua kuna wachache wanaweza wasitokee.”
Msimu uliopita Ligi Kuu ilianza na waamuzi wa kati 32 waamuzi wasaidizi 42 na wenye beji ya FIFA sita (kati) na waamuzi wa pembeni tisa.
Hamduni amesema wameomba kuongezea idadi ya waamuzi wenye beji ya FIFA kuwa 20 kati yao 10 waamuzi wa kati, ili iweze kuongeza ushindani kwa waamuzi.