Mamia ya raia wa eneo la Goma, wameandamana na kusababisha shughuli nyingi kusimama katika mji huo mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini uliopo mashariki mwa DRC, wakipinga kutokujali kwa jeshi la Afrika Mashariki lililowekwa katika eneo hilo ili kuwakabili waasi wa M23.
Raia hao wamesema, wameamua kuandamana ili kupinga Kikosi hicho cha kikanda cha Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC ambacho wanadai kiliingia nchini humo ili kuwaondoa m23, na kwamba hali ipo tofauti kwani waasi hao wameendelea kutamba bila upinzani.
Mmoja wa waandamanaji na mwanachama wa vuguvugu la wananchi la Mapambano ya Mabadiliko – LUCHA, Sankara Bin Kartumwa amesema, “tunachokiona sicho tulichokitarajia, hawa EAC walikuja hapa kupigana na M23 lakini hakuna dalili ya usaidia raia wanapoteana na wengine wanakufa na hali ni ileile.”
Aidha, amesisitiza kuwa, “kikosi hiki lazima kichukue hatua dhidi ya M23 kundi la waasi wengi wao kutoka jamii ya Kitutsi ambalo limeteka maeneo makubwa ya kaskazini mwa Goma katika miezi ya hivi karibuni na linaendelea kusonga mbele, ni lazima waanzishe mashambulizi na kuwafukuza M23 na washirika wao kutoka Rwanda.”
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono wanamgambo waasi wa M23, madai ambayo yanaungwa mkono na wataalamu wa Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi, ingawa Rwanda inayakanusha.