Mabingwa wa Soka nchini England ‘Manchester City’ wapo tayari kumuuza kiungo wa kimataifa wa Ureno, Bernado Silva katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa timu inayomhitaji itatoa kati ya Pauni 45 milioni hadi Pauni 50 milioni.
Inaelezwa kuwa mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 28 amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na FC Barcelona na Paris St-Germain (PSG) tangu dirisha lililopita la usajili barani Ulaya.
Silva kwa sasa anapokea mshahara wa Pauni 150,000 kwa juma na baadhi ya timu kubwa katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia zimeonyesha nia ya kutaka kumlipa mara mbili zaidi ya mshahara huo ili aende akakiwashe.
Hii inaonekana kuweka ugumu kwa Barcelona na PSG ambazo haziwezi kushindana katika suala la mishahahra dhidi ya timu za Saudia, ambazo tangu zianze kuwanasa nyota kutoka ligi mbalimbali Ulaya zimekuwa zikimwaga mkwanja wa maana.
Nyota huyu amebakisha mkataba wa miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa na anadaiwa kuwa ameomba kuondoka ili kupata changamoto mpya katika timu nyingine baada ya kuwa na misimu bora katika kikosi cha Manchester City ambako ni miongoni mwa wachezaji wachache wanaoheshimika na walioweka rekodi mbalimbali tamu katika Ligi Kuu England katika msimu uliopita, Silva alicheza mechi 55.