Klabu ya Azam FC imefikia makubaliano na vigogo wa Israel, Maccabi Tel-Aviv ya kumuuza kiungo chipukizi, Novatus Dismas.
Dismas anajiunga na timu hiyo baada ya Maccabi kuvutiwa na uwezo wake kwa kipindi cha takribani cha mwezi mmoja alichofanya majaribio ndani ya timu hiyo, ambayo imekuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).
Novatus anakuwa mchezaji wa pili kuuzwa na Azam FC msimu hu, baada ya wiki chache zilizopita kumpiga bei mshambuliaji Shaaban Chilunda, aliyejiunga na Mouloudia d’Oujda ya Morocco.
Mchezaji huyo bora chipukizi wa VPL msimu uliopita, amekuzwa kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC sambamba na Chilunda kabla ya wote kupandishwa timu kubwa kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo Azam FC imesisitiza kuendelea kuthamini na kuendeleza vipaji vya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cheo, na hawatasita kufanikisha ndoto zao za kwenda kucheza nje ya nchi pale mchezaji anapopata timu na taratibu zote zitakapofuatwa na timu husika.
kwa kuonyesha wamethamini na wataukumbuka mchango wake, uongozi wa Azam FC umeweka picha ya shukran kwa Novatus Dismas kwenye kurasa zao zote za mitandao ya kijamii.