Wabunge nchini Benin wamepiga kura kuhalalisha utoaji mimba na kuongeza wigo wa jambo hilo ambalo tayari lilikuwa likifanyika.
Wanawake sasa wanaweza kutoa mimba katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito iwapo kama ujauzito huo utamsababishia shida katika masuala ya elimu, kazi, maadili au mtoto anaweza kuathiri maisha ya mama au kwa ajili ya maslahi ya mtoto.
Katika nchi hiyo kabla ya utoaji wa mimba ulikuwa unaruhusiwa kisheria endapo mwanamke alibakwa au maisha ya mama yalikuwa hatarini kwasababu ya ujauzito.
Sheria mpya , ilipitishwa Jumatano usiku baada ya majadiliano makali bungeni , lakini bado katiba inapaswa kupitishwa mahakamani kabla ya utekelezaji kuanza.
Waziri wa afya Benjamin Hounkpatin ameunga mkono sheria mpya hiyo na kusema itaweza kuleta ahueni kwa wanawake wengi ambao wanapata ujauzito wasioutaka na hivyo kutafuta njia hatari zinazohatarisha maisha yao ili kutoa mimba.