Rais wa Kenya, William Ruto amewatahadharisha Wabunge kutoupinga muswada wake wa Fedha 2023 hadharani, mara utakapowasilishwa Bungeni wiki hii, huku akitishia kuwakabili wote watakaokiuka.
Akihutubu wakati wa hafla ya kurudisha shukrani kwa Waziri wa Mazingira, Soipan Tuya katika eneo la Leshuta, Narok Magharibi, Dkt Ruto alisema kuwa kura ya wazi itamsaidia kubaini wabunge wanaopinga ajenda yake ya maendeleo.
Amesema, “nilimsikia mbunge fulani akisema kuwa anataka kura hiyo kuwa ya wazi, ninaunga mkono wazo hilo. Nataka Wakenya wawajue viongozi ambao wanapinga juhudi zangu kuondoa ukosefu wa ajira. Wale watakaopinga mswada huo ni maadui wa maendeleo.”
Aidha, ameongeza kuwa, “mimi nangoja kuona mbunge ambaye atapinga mpango tulio nao na atasimama upande gani wa hawa wananchi. Nawarai wabunge kuupitisha Mswada wa Fedha wa 2023 pamoja na Hazina ya Ujenzi kwani ni mzuri kwa Wakenya.”