Kocha Mkuu mpya wa Azam FC, Youssouph Dabo ameweka wazi ratiba ya mazoezi kwa wachezaji wake ambapo sasa watakuwa wakifanya mara mbili kwa siku ili kujiandaa vyema na msimu mpya wa Ligi Kuu na Michauno ya Kimataifa.
Kikosi cha Azam FC Jumatano (julai 05) kilianza rasmi maandalizi ya msimu mpya wa 2023/24 wa Ligi Kuu Tanzania na michuano ya kimataifa kwa kufanya mazoezi mara moja asubuhi pekee lakini sasa kimeanza kufanya mara mbili kwa siku.
Kocha Dabo amesema watakuwa na vipindi viwili vya mazoezi asubuhi na jioni kwa muda wote wa maandalizi yao ambapo amegawa kwa asubuhi kuanga- lia utimamu wa mwili kwa wachezaji wake na jioni kufanya mazoezi ya kiufundi pamoja na kuchezea mpira.
Amesema anachokifanya ni kuwajenga wachezaji wake kuwa na nguvu lakini pia kuwa wanyumbulikaji wanapokuwa na mpira.
“Katika mchezo wachezaji watafanya makosa kwangu sio tatizo, kubwa ni kuwa na tahadhari na kufanyia kazi kila kosa tunaloliona uwanjani, wachezaji wako vizuri na kulingana na usajili uliofanyika na maandalizi tutafanya vizuri msimu ujao, ni naamini hivyo” amesema Dabo.
Amesema mikakati yao ni kuona wanaanda timu itakayokuwa na ushindani na kutoa changamoto kwa timu nyingine kwenye ligi msimu ujao na kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kutwaa ubingwa.
Katika hatua nyingine Beki Mpya wa Azam FC raia wa Senegal, Cheikh Tidiane Sidibe amesema anafurahi kuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC atahakikisha atashirikiana vyema na wachezaji wenzake kufikia malengo yaliyowekwa na klabu.
“Nina imani kubwa na kiwango changu, nitafanya vizuri na kuisaidia timu yangu kufikia malengo yanayotarajiwa kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, kikubwa ni kufuata yale maelekezo tutakayopewa na benchi la ufundi ili kufanya vizuri katika kila mchezo,” amesema Sidibe.
Kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka nchini Jumapili kesho kuelekea nchini Tunisia katika mji wa Sousse aliozaliwa na kuishi aliyekuwa kocha wa Young Africans, Nasreddine Nabi kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.