Wachezaji wa KMC FC wanatarajiwa kurejea kambini Machi 19, tayari kwa maandalizi ya michezo inayofuata ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo wamedhamiria kushinda ili kumaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi hiyo.
KMC ambayo imebakiwa na michezo mitano kumaliza msimu huu, itacheza dhidi ya Geita Gold FC, Dodoma Jiji FC, Singida Big Stars, Tanzania Prisons na Mbeya City. Michezo miwili kati ya hiyo itacheza nyumbani Uwanja wa Uhuru, Dar, tatu ni za ugenini.
Mwishoni mwa juma lililopita Kikosi cha Klabu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, kilifanikiwa kuichapa Kagera Sugar 2-0, katika Uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam na kufikisha alama 26 zinazoiweka kwenye nafasi ya 12.
Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala, amesema: “Tumewapa wachezaji wetu mapumziko ya siku 10 ili wakajiandae vema kumaliza msimu.”
“Tulipita kwenye kipindi kigumu ambacho hatukuwa na matokeo rafiki, Alhamisi ya juma lililopita tulifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar ambao umetupa morali ya kujipanga upya tutakaporejea mazoezini.”
“Ukiangalia ligi ni ngumu na timu zote zilizopo hivi sasa kila mmoja anataka kupata matokeo mazuri, hivyo kama tutarudi tukiwa na nguvu, hali na morali nzuri basi tutafanikiwa kumaliza msimu tukiwa kwenye nafasi nzuri.”