Baada ya kushuhudia kutojituma ipasavyo katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya lvory Coast juzi Jumamosi (Novemba 25) , Uongozi wa Simba SC umetangaza hali ya hatari kwa wachezaji wao.

Simba SC ililazimishwa sare ya bao 1-1 katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, hukU wachezaji karibu wote wakionekana kutokuwa fiti vya kutosha kuhimili mikikimikiki ya wapinzani wao hao, ambao walikuwa wakikimbia vema kwa dakika zote 90.

Baada ya mchezo huo, uongozi ulikutana na wachezaji na kuwaeleza kutoridhishwa na kiwango na morali ya timu katika mechi hiyo.

Taarifa kutoka Simba SC zinaeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah ‘Try Again’, alitaka kujua tatizo kutokana na kutocheza kwa kiwango kizuri.

“Viongozi kwa pamoja wametoa angalizo kwa wachezaji na kuwaambia kama mtu anajiona hawezi kuitumikia timu hiyo basi aweke wazi ili kupewa chake na kusepa,” amesema mtoa habari huyo.

Ameongeza kuwa baada ya mchezo huo wachezaji hawakuruhusiwa kwenda nyumbani na wote kutakiwa kuingia kambini na Alhamisi kuondoka kuelekea nchini Botswana katika mchezo wa pili wa Kundi B dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Kuhusu kocha mpya, Abdelhak Benchikha, amesema kuna mambo mawili kuwa anaweza kutua nchini leo au kwenda moja kwa moja Botswana kuunga na timu hiyo.

Katika hatua nyingine, Kaimu Kocha Mkuu, Daniel Cadena, amesema hajafurahishwa na sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya Asec Mimosas kwenye uwanja wa nyumbani malengo yao yalikuwa ni kukusanya pointi tatu Benjamin Mkapa.

Amesema walianza vema mchezo na kupata bao la Uongozi, kipindi cha pili hawakucheza vizuri wakaruhusu bao, lakini wameyapokea matokeo hayo kwani ndivyo mpira ulivyo.

Amesema wanasahau matokeo yaliyopita sasa wanaangalia mchezo ujao wanaoenda kucheza ugenini, lakini ujio wa kocha mkuu anaamini kila kitu kinakwenda kubadilika.

Wachezaji Chelsea wabebeshwa zigo
Wanawake changamkieni fursa kiuchumi - Katambi