Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira amesema uwepo wa nyota kama Clatous Chama, Saidi Ntibanzokiza, Kibu Dennis pamoja na wachezaji wengine wote unampa nguvu ya kuamua nani ataanza kikosi cha kwanza na kupata matokeo.
Ni dakika 1,710 ambazo ni michezo 19 mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara akishirikiana na Kocha mzawa Juma Mgunda wamecheza bila kufungwa baada ya kupoteza dhidi ya Azam FC walipofungwa bao 1-0.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kocha huyo kutoka nchini Brazil amekiongoza kikosi hicho kupata ushindi dhidi ya Wydad AC ambao ni mabingwa watetezi.
Ikiwa na mtaji wa bao moja kibindoni inatarajiwa kucheza na Wydad AC keshokutwa Ijumaa (Aprili 28) nchini Morocco kwenye Uwanja wa Mohamed V.
Oliveira amesema kuwa kuna wachezaji wazuri kwenye kikosi cha Simba ambao wanafuata maelekezo wanayopewa jambo linalompa furaha.
“Ninafurahi kuwa ndani ya Simba kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa ikiwa ni pamoja na Clatous Chama, Saidi Ntibanzokiza, Jean Baleke, Kibu Dennis, Mohamed Hussein, Joash Onyango.”
“Wote wanacheza kwa ushirikiano na hili ni jambo la muhimu kwetu kuona tunapata matokeo mazuri na kushinda mechi ambazo tunacheza tunaamini tutafanya vizuri kwenye mechi zetu ambazo zinatukabali,” amesema Oliveira.