Serikali Nchini, imeombwa kuboresha huduma ya upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika katika maeneo ya migodi, sambamba na kupeleka huduma ya mawasiliano katika kijiji cha Epanko kilichopo Halmashauri ya Mji Mahenge Wilayani Ulanga Morogoro, ili kurahisisha mawasiliano katika uendeshaji shughuli za uchimbaji madini ya vito (Spinel).
Ombi hilo limetolewa na Meneja Mgodi Elias Thomas baada ya kutembelea mgodi wa Franone Mining and Gems unaozalisha madini hayo na kusema kumekuwepo na changamoto ya mawasiliano ya simu za mkononi kwani mtandao uliopo ni mmoja pekee na unapatikana kwa shida.
Kuhusu kukatika katika kwa umeme hasa katika maeneo ya migodi, Thomas amesema hali hiyo inachangia kuendesha uzalishaji kwa hasara na Serikali pia kukosa mapato ambapo ameomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha maeneo yote ya migodi yanakuwa na umeme wa uhakika.
“Mgodi umetoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 lakini pia tumekuwa tukichangia uchumi wa nchi kwa ulipaji wa kodi lakini tatizo kubwa ni mawasiliano na umeme wa uhakika maana hali hii hupelekea kutokuwa na uhakika wa ufanyaji kazi hii changamoto kubwa tunaiomba Serikali itusaidie,” amesema Thomas.