Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ameagiza kukamatwa wadaiwa sugu wa makusanyo ya Mapato ya ndani shilingi Milioni 48 na kuhakikisha wanarejesha fedha hizo ndani ya mwezi mmoja Wilayani Misungwi.
Mhandisi Gabriel ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo lililofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri kwa ajili ya kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Amewataka Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuhakikisha Watumishi hao wanaodaiwa fedha hizo wanarejesha mapema fedha za Serikali ambapo waangalie pia mikataba yao na kuona Wadhamini wao ili waweze kutoa fedha za makusanyo ya mapato ya ndani wanayodaiwa ili ziweze kutumika kuleta maendeleo kwa Wananchi wa Misungwi.
Amesema kwamba fedha za mapato ya ndani shilingi 48,316,205/= zilizokusanywa kwa nyakati tofauti na Wakusanya mapato wa Halmashauri hiyo wakiwemo Watumishi na wakusanyaji wengine wa mapato walioingia mikataba ya kukusanya mapato husika.
“Lazima msome tabia za wakala wanaokusanya fedha za mapato na kujiridhisha na uhalali na nyendo zao na kuhakikisha wanajiridhisha fedha za mapato kwa wakati,” amesisitiza Mhandisi Gabriel.
Ameeleza kuwa vyombo vya uchunguzi wawasake wote na warejeshe fedha zote za makusanyo ya mapato ya ndani na kuwataka Watumishi wote wanaodaiwa fedha za mapato wakatwe kutoka katika mishahara yao pia wajiridhirishe katika kudhibiti fedha za mapato yasivuje na kuimarisha mifumo na kuweka mikataba makini na kuagiza suala hilo lishughulikiwe kwa wakati ndani ya mwezi mmoja.
Kwa upande wake Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi limeridhiria agizo hilo la Mkuu wa Mkoa la kuwakamata wadaiwa sugu wa makusanyo ya fedha za mapato pamoja Wadaiwa wa madeni ya mikopo ya Vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu ambazo ni fedha za Vikundi shilingi milioni 83.9 ambazo walikopeswa kwa muda lakini hawajweza kurejesha fedha hizo kwa wakati.
Awali akiwasilisha taarifa ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Benson Mihayo amesema kwamba katika ukaguzi huo Halmashauri hiyo imepata Hati ya kuridhisha ambapo hoja zilizohojiwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 zinaendelea kutekelezwa.