Katika kudhibiti wakopaji wasumbufu, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kushirikiana na Dun & Bradstreet Credit Bureau Tanzania Ltd. imezindua rasmi kanzidata itakayowezesha upatikanaji wa taarifa za fedha kwa wakopaji kwa lengo la kuwatambua wafanyabiashara wanaokopa na kushindwa kurejesha kwa wakati.
Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa fedha kutoka BOT, Jerry Sabi amesema mfumo huo ni mapinduzi mapya ya kuwawezesha taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wingi.
Amesema BoT imeshatoa leseni kwa kampuni hiyo ili kuchakata taarifa za wakopaji kutoka kwenye kanzidata ya Benki Kuu.
Aidha, Afisa Mkuu Mtendaji wa Dun & Bradstreet Credit Bureau, Miguel Llenas amesema kuwa mfumo huo utasaidia benki na taasisi zinazotoa mikopo kuwatambua wakopaji wasumbufu na kupunguza mikopo.
Ameongezea kuwa mfumo huo utaongeza uwajibikaji katika kukopesha na kukopa, pia utasaidia wakopeshaji na wadai kusimamia vitabu vyao vya mkopo na kuhakikisha viwango vya riba hulingana na maelezo husika ya mkopaji na kukuza bidhaa za mkopo katika soko la wakopeshaji.
“Pia inapunguza muda wa kupata mkopo kulingana na taarifa za mkopo zilizopo kwenye ripoti zake hivyo kukuwezesha kama dhamana ya mkopo wako mpya na kukupatia mkataba bora na wenye kiwango stahiki cha riba.
“Inampa mkopeshaji taarifa sahihi za mchakato wa utoaji wa mikopo; ujumbe na mwongozo wa tathmini ya mkopaji, pia kuwezesha kasi ya utoaji mkopo na usimamizi wa wateja husika.
“Pia mtoaji wa huduma anaweza kuongeza kasi ya upatikanaji wa wateja, kuelekeza na kusimamia mipaka ya mkopo yao na kuboresha utoaji wa huduma hizo.
Akifafanua zaidi kuhusu huduma hizo, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Adebowale Atobatele alisema lengo lao kila wakati limekuwa kutoa suluhisho la usimamizi kuelekea mikopo isiyolipika katika sekta mbalimbali na kutoa taarifa sahihi kwa watoa mikopo kufanya maamuzi sahihi ya kutoa au kutokutoa mikopo.
“Lakini pia kuharakisha kasi yao ya kuchukua maamuzi; kurahisishaji upatikanaji wa haraka wa bidhaa za mikopo kwa kampuni zinazostahiki, watu binafsi na hivyo kukuza fursa za ukuaji kwa uchumi kwa wote.
“Pia tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote na wahusika wote nchini ili kusaidia kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za mkopo nchini, “alisema.
Alisema kanzidata hiyo itakuwa na taarifa za kihesabu ambazo wakopeshaji hutumia, pamoja na ripoti ya mkopo kutathmini hatari ya kutoa mkopo.
“Mfumo huu ni njia muhimu za kukopesha ambayo inaweza kuamua ikiwa unapata mkopo, viwango gani vya riba unalipa kwa deni husika, “alisema.
Naye Ofisa Mkuu wa masuala ya Ufundi wa kampuni hiyo, Kelyn Pena alisema mfumo huo kwa watumiaji wa kampuni hiyo wa kipekee nchini Tanzania kwa sababu inatoa taarifa halisi za kitakwimu.
“Kanzidata hii ni rahisi kutumiwa na taasisi za kifedha na watumiaji kwa jumla kwani iko thabiti katika mpangilio wa wakati na utofauti wa historia ya mikopo ya watumiaji. ” alisema