Wadau mbalimbali wa masuala ya Afya, wamesema hawashangazwi na ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, juu ya ongezeko la watu wenye ugonjwa wa Kisukari na badala yake wameshauri kuwekwa kwa mikakati ya kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo hasa kwa bara la Afrika linaloonekana kuwa na changamoto kubwa ya tatizo hilo.
Hatua hiyo, inafuatia takwimu zilizotolewa na WHO kanda ya Afrika Novemba 14, 2022 nilizoonesha kiwango cha changamoto ya ugonjwa wa kisukari Afrika kuwa ni kikubwa ambapo watu wazima wapatao milioni 24 walioathiriwa na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 129 hadi kufikia watu million 55 ifikapo mwaka 2045.
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti alisema, “Mwaka jana ugonjwa wa kisukari ulikatili maisha ya watu 416,000 barani Afrika na ugonjwa huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya vifo Afrika ifikapo mwaka 2030. La msingi zaidi ni kwamba kisukari ndio ugonjwaa pekee usio wa kuambukiza ambao hatari yake ya vifo vya mapema inaongezeka badala ya kupungua.”
Wadau hao, wamesema ni vyema kuudhibiti ugonjwa huo mapema na bila usimamizi na mabadiliko ya mwenendo wa maisha, kisukari kinaweza kusababisha matatizo mengine mengi yakiwemo magonjwa ya mshtuko wa moyo, kiharusi, figo kushindwa kufanyakazi, kukatwa kwa viungo vya mwili kama miguu, ulemavu wa kutoona, upofu, na uharibifu wa mishipa.
Aidha wameongeza kuwa, ili kuharakisha hatua za kuudhibiti ugonjwa wa kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza, ni vyema WHO ikajielekeza katika mikakati ya utoaji wa elimu kwa Watu ikiwa na lengo la kupunguza athari za ugonjwa huo, na kuhakikisha kwamba kila mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari anapata matibabu yenye ubora.