Mfanyakazi mmoja wa Benki ya NMB amefariki dunia na wengine kumi wamenusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wamepanda kuzama ndani ya Bahari ya Hindi, eneo la Raskazone jijini Tanga.
Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita, wafanyakazi hao walipokuwa wakisafiri kuelekea Kisiwa cha Toteni kwa ajili ya kufanya utalii.
Meneja wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Christopher Mlelwa alimtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Patrick Kiunguli mwenye umri wa miaka 53. Alisema mwili wake ulipatikana kutokana na juhudi za uokoaji zilizofanywa na kikosi cha maji cha Jeshi la Wananchi.
Kikosi hicho cha Jeshi la Wananchi kilishirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wazamiaji majini wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
“Hawa wafanyakazi walikuwa wakienda Kisiwa cha Toteni kufanya utalii ikiwa ni sehemu ya kusherehekea siku ya familia ya wana NMB. Lakini walipofika katikati boti ilipigwa na wimbi na kupinduka,” Mwananchi inamkariri Mlelwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa watu 10 kati ya 11 waliokuwa kwenye boti hiyo mali ya Klabu ya Yatchi waliokolewa kwa nyakati tofauti. Alisema mtu mmoja alifariki na mwili wake ulipatikana.
-
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 13, 2019
-
DJ Arafat afariki dunia kwa ajali ya pikipiki, daktari aeleza hali ilivyokuwa