Wapendanao Wilson na Salome Kufuna wamefanikisha azma yao ya kufunga ndoa katika kipindi hiki cha janga la corona, wakitumia njia ya mtandao kukamilisha mchakato wote wa kuwa mume na mke kisheria kufuatia zuio la mikusanyiko nchini Kenya.
Wilson na Salome wamekuwa wapendanao wa kwanza kufunga ndoa jana, Julai 10, 2020 kwa njia ya mtandao tangu Serikali ilipoanzisha huduma hiyo.
“Tulitumia mtandao kukamilisha hatua zote na tulifanikisha kwa ufasaha. Zilikuwa hatua rahisi, nyaraka zote kuzijaza zilichukua dakika chache,” alisema Bi. Harusi, Salome.
“Tuliwasilisha maombi yetu Juni 17 na jana tulipata mrejesho. Kisha tukawasilisha tarehe ya siku ya kufunga ndoa yetu na leo tumefunga ndoa. Tunafurahi tumepata vyeti vyetu vya ndoa ndani ya dakika 20 tu,” aliongeza.
Salome na Wilson walifika kwa Msajili baada ya kukamilisha taratibu zote, kwa lengo la kula kiapo cha ndoa. Wawili hao walionekana wakiwa wamevalia barakoa na kuendelea na utaratibu wa kujikinga na virusi vya corona kwa kumpa umbali wa kutosha Msajili.
Serikali ya Kenya ilisimamisha kwa muda shughuli zote za ufungishaji ndoa ili kupambana na virusi vya corona kwa kuepuka mikusanyiko. Hadi sasa Wizara imeeleza kuwa imeshapokea maombi 2,551 ya watu wanaotaka kufunga ndoa.
Imeelezwa kuwa mfumo huo wa kufunga ndoa mtandaoni ulianzishwa baada ya watu wengi kuandamana kwenye ofisi ya Msajili wakihitaji huduma ya kufunga ndoa.
DAS wa Handeni afariki kwenye ajali Dodoma, Mbunge ajeruhiwa