Wafungwa 150 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepelekwa katika Gereza la Kwitanga mkoani Kigoma ikiwa ni mkakati maalumu wa Serikali kuliteua gereza hilo kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la mchikichi nchini.
Hayo yamebainishwa leo na naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mkakati huo uliotolewa maagizo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati ya mwaka 2018 alipofanya ziara gerezani hapo ukiwa na lengo la kulifanya Jeshi la Magereza kuingia katika mfumo wa uzalishaji mali.
“Katika kutekeleza agizo la waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo ni agizo la serikali, wizara tumeongeza nguvukazi hapa kwa kuleta wafungwa 150 na muda si mrefu tutaongeza wafungwa wengine 300 kutoka magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuongeza uzalishaji huku eneo lenye ukubwa wa ekari 6000 linatarajiwa kulimwa zao hilo sambamba na kusambaza mbegu zinazozalishwa gerezani hapo kwenda Halmashauri za Mikoa, Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi,” amesema Masauni
Na kuongeza kuwa “Lakini pia ili kuliwezesha gereza hili tumeliagiza Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza kulichukua Gereza la Kwitanga na kuliingiza katika kundi la magereza yanayowezeshwa na shirika ili kuweza kutatuliwa matatizo yao ya kifedha badala ya kusubiri bajeti kuu kutoka serikalini ambayo inakua haitoshi”
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Magereza mkoani Kigoma, Kamishna Msaidizi Leonard Bushiri ameunga mkono hoja ya Gereza Kwitanga kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali huku akikiri baadhi ya masuala kukwama kutokana na changamoto za kibajeti.
“Nafikiri hili suala la gereza kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji mali litatatua changamoto nyingi za kibajeti na kiuendeshaji maana gereza halina gari kubwa kwa ajili ya uvunaji na usafirishaji wa mafuta kutoka gerezani kwenda kwa mtumiaji, hakuna bajeti ya uendeshaji kwa mfano kukamua lita 100 mpaka 120 za mafuta tunahitaji maji lita 1000 ” amesema ACP Bushiri.