Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amesema kuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyefukuzwa uanachama wa chama hicho, ana haki ya kufuata taratibu zinazoweza kumrejesha ndani ya chama hicho.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na magazeti ya Mwananchi na The Citizen, Dkt. Bashiru alieleza kuwa adhabu aliyopewa Membe kwa kawaida ni kubwa hivyo anayozungumza sasa yanaweza kuwa mambo yanayotokana na uzito wa adhabu, lakini akipata nafasi ya kushauriwa na kutulia huenda akabadilika.

“Unajua adhabu kubwa hii, Membe ana haki yake, anahitaji ushauri nasaha kwa sababu hili sio jambo dogo, asitapetate. Na mimi nisingetaka kulizungumza kwa ushabiki, hata lingenipata mimi nahitaji marafiki zangu wa karibu niwashirikishe, kama nina busara ya kutosha,” alisema Dkt. Bashiru.

Aidha, Katibu Mkuu huyo wa CCM alieleza kuwa Membe anayo nafasi ya kukata rufaa kwani mchakato uliompa adhabu ni sawa na mchakato wa kimahakama, hivyo kwa nafasi yake kwakuwa ndiye anayepaswa kuipokea rufaa yake si vyema akaingilia mchakato huo.

“Mchakato huu ni kama wa kimahakama, kuna rufaa. Sasa nikianza mimi kusema wakati mimi ndio nitapokea rufaa kama ipo ni kama naingilia mchakato wa haki,”

“Na mimi ndiye muandaaji wa ajenda ya rufaa. Tunaweza kupeleka jambo hili, Halmashari Kuu ikasema ‘msameheni’, kwasababu yenyewe ndiyo iliyosema ‘muite’,” aliongeza.

Hata hivyo, Dkt. Bashiru alisema kuwa kwakuwa yeye ndiye aliyewapokea baadhi ya viongozi waliokuwa wametoka kwenye chama hicho kwenda upinzani, huenda siku moja akampokea tena Membe kutokana na utaratibu wa mfumo wa vyama vya siasa. Aliongeza kuwa ameshasaini barua 14 za kuwasamehe wanachama wa chama hicho waliokuwa wameadhibiwa.

“Mimi ndiye niliyewapokea akina Lowassa [Edward], nimewapokea akina Sumaye [Frederick], akina Dkt. Slaa, sasa siku moja ninaweza kumpokea Membe. Sasa nikianza kubwabwaja hapa nitakuwa kama vile sina context,” alisema.

Akizungumzia sababu alizotoa Membe kuwa anafahamu amefukuzwa kutokana na sababu za kutaka kugombea nafasi ya Urais, Dkt. Bashiru alisema bado anaweza kuingia katika vyama vingine vya siasa na kuingia uwanjani kushindana na chama hicho.

“Kuhusu sababu ya urais aseme chochote tu lakini mimi siwezi kusema siri za vikao na michakato yake, lakini urais ndio nini… kwa sababu ukishafukuzwa kwenye chama cha CCM katiba haisemi hauwezi kugombea kwenye vyama 19 vilivyobaki, lakini ukifungwa ndiyo unaweza kukosa sifa. Sasa adhabu aliyopewa hazihusu sheria za nchi kumuondolea sifa za kuwa Rais. Aende na nguvu zake na wafuasi wake tukutane uwanjani na mwaka huu utakuwa mwaka mzuri sana, atakuwa bado ana nguvu tushindane naye kama ni Urais,” alisema Dkt. Bashiru.

Kamati Kuu ya chama hicho ilimfukuza uanachama Membe hivi karibuni, baada ya kuhojiwa na Kamati ya Udhibiti na Nidhamu ya chama hicho.

Wengine waliokuwa kwenye mchakato huo wa kuhojiwa ni Katibu Mkuu wa zamani, Abdulrahman Kinana ambaye alipewa karipio kali na Katimu Mkuu wa zamani, Yusufu Makamba ambaye alisamehewa.

 

Waziri mkuu Iraq ajiuzulu
Wafungwa 150 kulima Michikichi Kigoma

Comments

comments