Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali -CAG, imesema imebaini uwepo wa Wafungwa (Wahamiaji wasio na vibali), 3110 ambao waliomaliza vifungo vyao lakini bado wako Gerezani.
CAG Charles Kichere, ameyasema hayo wakati Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo jiji Dodoma, kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu ya ofisi yake ya mwaka 2021/2022.
Amesema, “katika ukaguzi nilibaini Idara ya Jeshi la Magereza ina Wahamiaji 4,419 haramu kutoka Nchi mbalimbali, huku 1,264 wakiendelea kutumikia vifungo, 45 wamewekwa Mahabusu na 3,110 wanaotakiwa kurejeshwa makwao.”
Aidha CAG ameongeza kuwa, “uwepo wa wafungwa ambao wamemaliza vifungo vyao lakini bado wako gerezani katika kipindi cha mwaka mmoja hadi mitano unatokana na kutokutolewa amri ya kuachiliwa huru na Wizara ya Mambo ya Ndani, gharama za kuwahudumia Wahamiaji hao ni kubwa na chakula cha Mfungwa mmoja kilitengewa bajeti ya Shilingi 5,000 kwa siku”
Hata hivyo ameongeza kuwa, “kitendo cha kuwa na Wahamiaji 3,110 katika magereza hayo huigharimu TSh. bilioni 5.68 kwa mwaka, hivyo kuipa mzigo Serikali, Idara ya Jeshi la Magereza imeitaka Idara ya Uhamiaji kuchukua hatua stahiki za kuwarejesha makwao Wahamiji wanaomaliza vifungo vyao ili kuepuka gharama za ziada.”
Hata hivyo, Kichere ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kufanya juhudi za kuhakikisha maagizo yanatolewa kikamilifu, ili kuwarejesha raia wa kigeni walioachiliwa huru nchini kwao ili kupunguza gharama zisizo za lazima.