Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini – TARURA, kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha wahandisi wazawa wanashiriki kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali nchini.
Majaliwa ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku Wahandisi, na kudai kuwa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Tanzania, unaolenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka 9% hadi 8% ifikapo 2025/26, Serikali inatarajia inazingatia ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya ujenzi, ili kukuza ujuzi.
Amesema, “Wizara ya Ujenzi pamoja na bodi ya wahandisi inalifanyia kazi suala la ushiriki mdogo wa wazawa katika miradi ya maendeleo, hii ni changamoto ambayo mmeiibua, Serikali sasa imeliweka kwenye mpango wa kuhakikisha changamoto inafanyiwa kazi ili kuongeza idadi ya wazawa kushiriki katika kazi za ndani.”
Hata hivyo, ameongeza kuwa, “Serikali imedhamiria kuhakikisha wahandisi wazawa wananufaika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali na miradi hii ni fursa kwenu, natoa rai mjipange na kufanya juhudi za makusudi kila mmoja kwenye eneo lake ahakikishe kwa uzalendo alionao na mapenzi kwa nchi yake kuwa kinara katika sekta unayosimamia ili kulijenga taifa letu.”