Watanzania wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo, ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, kupinga rushwa, kujituma na kuzidisha upendo miongoni mwa jamii.
Wito huo, umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango hii leo Oktoba 14, 2022 wakati akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Ibada maalum ya Kumuombea Baba wa Taifa iliyofanyika Kanisa Kuu Katoliki Mjini Bukoba, Kagera.
Amesema, katika kumuezi Hayati Baba wa Taifa ni lazima kuendeleza amani na umoja kwa watanzania na bara la Afrika kwa ujumla na kuwataka viongozi kufanya kazi kwa kutenda haki, uadilifu ili taifa liweze kupata wataalamu watakaotoa msaada kwa Taifa.
Makamu huyo wa Rais, pia ametoa wito kwa watanzania kutafuta hekima za Mwenyezi Mungu wakati wote wa kutekeleza majukumu kama alivyofanya Hayati Baba wa Taifa enzi za uhai wake na kwamba upendo na uadilifu miongoni mwa jamii utasaidia kuepusha migongano isiyo na ulazima.
Ibada maalum, ya Kumuombea Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere, imeongozwa na Askofu wa Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.