Raia nchini Pakistan, wamehimizwa kupunguza unywaji wa chai ili kustawisha uchumi wa Taifa hilo kutokana na sababu zilizotajwa kuwa nchi hiyo inaagiza chai kutoka nje kwa kukopa pesa.
Waziri wa Shirikisho la Mipango na Maendeleo, Ahsan Iqbal, amewaambia waandishi wa habari kwamba Wapakistani wanaweza kupunguza matumizi yao ya chai kwa kunywa kikombe kimoja au viwili kwa siku.
Nchi hiyo pia inaripotiwa kukabiliwa na changamoto za kiuchumi kwa miezi kadhaa, na akiba ya chini ya fedha za kigeni ikisababisha uhitaji wa kifedha wa haraka.
“Ninatoa wito kwa taifa kupunguza matumizi ya chai kwa vikombe kimoja hadi viwili kwa siku sababu tunaagiza chai kwa mkopo,” amesema Iqbal
Ombi hilo linajiri wakati akiba ya fedha za kigeni ya Pakistani inaendelea kushuka kwa kasi, na kuweka shinikizo kwa Serikali kupunguza gharama kubwa za kuagiza na kuhifadhi fedha nchini humo.