Katibu Mkuu Ofisi ya Mkamu wa Rais, Mary Maganga amewahimiza viongozi wote wanaosimamia Mradi wa Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi – NAP, kufanya kazi ipasavyo na kwa usahihi.
Ametoa wito huo wakati akiongoza kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya NAP cha mwaka cha kupitia taarifa za utekelezaji wa mradi kuanzia Aprili hadi Septemba, 2023.
Amesema, Viongozi hao kufanya kazi kwa kasi ili kukimbizana na muda huku akisisitiza kuwa katika kikao kijacho kila mmoja awe ametekeleza vyema majukumu yake kama ilivyokubalika.
“Kila jambo lina changamoto zake lakini hadi hapa tulipofika sasa tumeona mafanikio makubwa tangu tulipoanza utekelezaji wa mradi huu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema Bi. Maganga.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Asia Akule kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi unakwenda vyema na kwa mafanikio makubwa.
Mradi huo wa miaka mitatu ulianza kutekelezwa mwaka 2022 na utafikia tamati mwaka 2024 ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) inaendelea kutekeleza NAP.