Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NACTE), Dkt. Charles Msonde amesema kuwa wanafunzi wote ambao walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Sekondari nchini wanatakiwa kufanya mtihani wa udahili tarehe 28 mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka NECTA iliyotolewa na Edgar Kasuga kwa niaba ya katibu Mkuu kwenda kwa Makatibu Tawala wote Tanzania Bara siku ya Jumatatu, iliwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kidato cha kwanza kufanya mtihani wa kudahili ufaulu wao ili waweze kujinga kidato cha kwanza na wale amabo hawatafaulu hawataruhusiwa kuendelea na masomo hayo ya Sekondari.
NECTA inakusudia kutumia mtihani huo kuhakiki kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika Mtihani wa Taifa wa kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika mwaka jana.
Makatibu Tawala wote, maafisa elimu na waalimu wakuu wote wa shule za Sekondari za Serikali waliombwa kuwasilisha orodha ya majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule zao ili maandalizi yafanyike, taarifa rasmi kwa umma itatolewa endapo mabadiliko yeyote yatajitokeza.
Pia Takwimu fupi ilitolewa kuonesha kiwango cha ufaulu wa Elimu ya Msingi kwa mwaka jana, ambapo watoto 789,479 walifanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu Elimu ya Msingi , 555,291 walifaulu. Idadi hii ya ufaulu ni sawa na asilimia 70 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo.