Vita ya kupambana na dawa za kulevya nchini iliyopamba moto zaidi na kuzua mijadala tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipoanza kutaja majina ya watuhumiwa imemuibua Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dkt. Wilbroad Slaa.

Dkt. Slaa ameibuka baada ya kutajwa na kuhojiwa kwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye alikuwa rafiki yake na ‘muwezeshaji’ wake kabla siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 hazijawageuza kuwa mahasimu.

Akizungumza jana kanisani kwake wakati akiwasimulia waumini wake mkasa uliompata tangu alipowasili katika kituo cha kati cha polisi jijini Dar es Salaam hadi alipoachiwa, Askofu Gwajima alisema kuwa alipokea ujumbe wa Dk. Slaa ambaye alimtetea dhidi ya tuhuma hizo.

Aidha, Gwajima alimpinga vikali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akidai kuwa ni kombora ambalo linaweza kutua sehemu yoyote.

“Mheshimiwa Rais, Makonda ni kombora ambalo halijaelekezwa mahali pa kutua, linaweza kutua popote hata chumbani na kama ataendelea kuwa mkuu wa mkoa, mimi sikubali, mimi sikubali,” Gwajima anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliwataka watanzania wote kuunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya bila kujali uongozi wa dini, siasa au umri wa mtu, huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akitarajiwa kutangaza orodha nyingine ya watuhumiwa mapema leo.

Wahitimu darasa la saba kuchujwa upya kujiunga kidato cha kwanza
Video: JPM achukizwa mzaha vita dawa za kulevya, Gwajima afunguka...