Jumla ya pampu tatu za kusukuma maji, ambazo hutumika kuchepusha maji kutoka mto Ruvu unaotegemewa na wakazi wa jijini Dar es Salaam na Pwani zimekamatwa baada ya kufanyika kwa ukaguzi uliofanywa na bodi ya maji Bonde la Wami/Ruvu.
Kiongozi wa operesheni kutoka bonde la Wami/Ruvu, Mshuda Wilson amesema ni vyema wananchi kufuata maagizo yanayotolewa na bodi kwa matumizi ya maji kama kuomba vibali kwani vibali vinapatikana wafuate utaratibu ili waweze kufanya shughuli zao kihalali.
Amesema, ukaguzi huo umefanyika katika maeneo tofauti ya vyanzo vya maji kwa lengo la kuwaondosha na kuwapa elimu wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa vyanzo vya maji kinyume na kifungu cha 64 (1) (a-c), cha sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji, Sura ya 331.
Wananchi hao, waliopo katika kijiji cha Madege kata ya Duthumi wilaya ya Kibaha hutumia ‘pampu’ za kusukuma maji katika mashamba yao, pamoja na kuuuza kwa wanachi wengine bila ya kuwa na kibali cha matumizi ya maji kinachotolewa na mamlaka.
Operesheni iliyofanyika vitongoji vya Kihumbageni na Kisaki kituoni, bodi ilifanikiwa kukamata pampu nne za kusukuma maji, wafugaji watatu waliokuwa wakipeleka mifugo katika vyanzo vya maji na mkulima mmoja aliyekuwa hana kibali cha matumizi ya maji kutoka bonde la Wami/Ruvu.
Pamoja na matukio hayo, pia zoezi la utolewaji wa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa viongozi wa vijiji lilifanywa na Timu ya operesheni, ili viongozi waweze kufikisha ujumbe kwa wananchi kufuata kanuni, taratibu na sheria ya matumizi ya maji.