Waislamu nchini wametakiwa kuongeza kufanya ibada ikiwemo nyakati za usiku katika kipindi hiki cha kumi la mwisho ili kujikurubisha zaidi kwa mola wao.
Hayo yamebainishwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shehe Saleh Kabi wakati akizungumza na waumini katika msikiti wa Mazizini katika kipindi cha darasa kwa waumini.
Amesema fadhila za mwezi huu ni nyingi ikiwemo kushushwa kwa usiku wenye utakatifu mkubwa wa baraka nyingi wa Lailatul – kadri.
“Waislamu hili ni kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo miongoni mwa sifa zake kubwa ni waumini kufanya ibada kwa wingi nyakati za usiku na kujikurubisha kwa mola mtukufu ili kupata pepo na kufutiwa madhambi yao” amesema Mufti Kabi.
Aidha ametoa wito kwa waislamu kuchukua nafasi ya kuliombea dua taifa la Tanzania pamoja na ulimwengu kwa ujumla kuondokana na janga la ugonjwa wa covid – 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.