Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka Wakandarasi wanaojenga miradi ya barabara nchini kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana hususan katika kipindi cha kiangazi ili kipindi cha masika kinachosababishaga miradi mingi kusimama.
Naibu Kasekenya ameyasema hayo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi wa barabara ya Kabingo- Kasulu- Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.
“Nimepita kuangalia maendeleo ya mradi huu wa barabara yenye urefu wa kilometa 260 ambao unatekelezwa na makandarasi mbalimbali katika vipande vinne tofauti, nimefurahishwa na baadhi ya makandarasi hawa kujiongeza kwa kuamua kuongeza muda wa ufanyaji kazi, hii itasaidia hata miradi kukamilika kwa wakati, hivyo nawaagiza makandarasi wengine nao kuiga mfano huu”, Amesema Kasekenya.
Aidha amewasisitiza Makandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kubainisha changamoto zozote zinazowakabili ili zitatuliwe mapema wakati mradi ukiwa kwenye hatua za awali, pia amewahakikishia Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha miradi haikwami kutokana na ucheleweshaji wa malipo.
Wakati akimalizia ziara yake wilayani Kibondo mkoani humo, akiwa anakagua kipande cha Tatu cha barabara cha Mvugwe – Nduta Junction (Km 59.35), amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza muda wa safari kutoka wilayani hapo kuelekea mikoa mingine kama vile Mwanza, Kagera na nchi jirani ya Burundi.