Mahakama Kuu ya Shirikisho ya jijini Lagos nchini Nigeria, imekataa kusikiliza kesi zilizowasilishwa na Wakili wa Haki za Binadamu, Malcolm Omirhobo baada ya kufika mbele ya Mahakama hiyo akiwa amevalia mavazi yanayodaiwa kuwa na mfanano na Waganga wa jadi.
Wakili Omirhobo, anadaiwa kutenda tukio hilo Juni 27, 2022 wakati alipowasili katika Mahakama hiyo ya Juu, akiwa na mchoro wa chaki nyeupe uliozunguka jicho lake moja huku akijifunga minyororo kwenye miguu, kufunga kitambaa chekundu kiunoni mwake na kuvaa manyoya kichwani.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama Kuu ya Shirikisho, Tijani Ringim akiwa amevalia mavazi hayo Omirhobo alizua hisia tofauti kutoka kwa baadhi ya mawakili waliodai kuwa hangeweza kusikiliza vyema shauri lake, kitu ambacho kilizua mabishano kwa muda akidai alikuwa nadhifu.
Kesi ya kwanza ya Omirhobo, ilikuwa ni ile dhidi ya Serikali ya Shirikisho ya Nigeria na nyinginezo huku shitaka la pili likiwa dhidi ya Jeshi la Nigeria na watu wengine wawili, ambapo iliitishwa na Jaji kisha kukataliwa kusikilizwa na kuahirishwa kitendo alichokiita ni uvunjifu wa haki.
“Bwana wangu, sheria haziwezi kuchukua nafasi ya Katiba ya Shirikisho la Jamhuri ya Nigeria, sionib tatizo juu ya mavazi niliyovalia maana hayana uhusiano wowote na usikilizwaji wa kesi hii ukizingatia nipo nadhifu sasa kwanini kuna hisia tofauti,” amehoji Omirhobo.
Mara baada ya kusikiliza hoja yake, Hakimu Ringim alimuagiza Omirhobo azungumze mbele ya Mahakamani kwa nini kesi yake isisikilizwe kutokana na jinsi alivyovalia katika tarehe tarehe ya kesi yake, ambapo mara baada ya utetezi Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, 2022.
“Huwezi kuhutubia Mahakama kama hii kama mtaalamu, na hata utetezi wa hoja zako bado hazina mashiko kikanuni hivyo nitaahirisha kesi yako na wewe njoo uhutubie korti ikiwa kanuni zitakuruhusu kufika kortini ukiwa na mavazi ya namna hii,” Hakimu Kiongozi alisema.
Juni 17, 2022, Mahakama hiyo ya juu ilitoa idhini kwa wanafunzi wa kike Waislamu kuvaa hijab shuleni katika Jimbo la Lagos, ambapo baadhi ya wajumbe watano kati ya saba wa jopo la mahakama hiyo walioketi kwenye kesi waliamua kuunga mkono huku wajumbe wawili waliosalia wakipinga.
Siku ya kesi, Wakili Malcom akaonekana akiwa amevalia vazi kamili la kitamaduni la ‘kasisi wa Olokun’ Mahakamani na kuwaambia Wanahabari kuwa alikuwa akitumia haki zake za kimsingi kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoidhinisha uvaaji wa hijabu shuleni.
Malcom alisema, maana ya hukumu hiyo ni kuwa kila Mnigeria ikiwa ni pamoja na Madaktari, Polisi, Wanafunzi wa kijeshi na Waandishi wa habari sasa wanaweza kuvaa mtindo wao wa wa mavazi wanaodhani upo sawa bila kuvunja sheria katika maeneo ya umma.
Aidha, akabainisha kuwa hapingani na hukumu iliyotolewa bali alifurahishwa na uamuzi huo kwa sababu uliimarisha haki za Wanigeria wote kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Shirikisho la Jamhuri ya Nigeria ya 1999 iliyorekebishwa.
Wakati huo huo, Mwanasheria mmoja Ahmad Adetola-Kazeem, ambaye hakuonekana kufurahishwa na uvaaji wa Wakili Malcolm, alikashifu hatua za wakili wa haki za binadamu kwa kutoa vazi la kitamaduni mahakamani, akidai lilikuwa ni jaribio la makusudi la kukejeli na kuiaibisha Mahakama kitu ambacho kimepingwa na baadhi ya watu.