Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa, linamshikilia mtu mmoja Tanda Thadeo (30), kwa tuhuma za kuwatumia wanafunzi kushiriki zoezi la kufukua kaburi la mtoto ili afufuliwe.

Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa, ACP Theopita Mallya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusemsa mtuhumiwa ni mkazi wa kitongoji cha Kasisiwe kilichopo manispaa ya Sumbawanga.

Amesema, Thadeo anashikiliwa kwa tuhuma za kuwatumia wanafunzi hao wa Darasa la sita katika Shule ya Msingi Kasisiwe iliyopo Manispaa ya Sumbawanga, kwa kuwaahidi ya malipo ya shilingi elfu kumi.

“Mtuhumiwa alifanya tukio hilo ikidaiwa kuwa wanataka kumfufua mwanae na tayari tumeitembelea shule hiyo ili kutoa elimu kwa wanafunzi juu ya kutambua matendo ya kihalifu, na watoto waliofanya kazi hii walipewa ahadi ya malipo ya shilingi elfu kumi,” amesema Kamanda Mallya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi wilaya ya Sumbawanga, Marry Kway naye alishiriki katika kutoa somo la ukatili wa kijinsia na namna ya kuripoti matukio ya kihalifu kwa wanafunzi wa shule hiyo, ili kupunguza vitendo vya uvunjifu wa amani kwa jamii.

Mtoto huyo Martine Tanda (2), anayedaiwa kutaka kufufuliwa alifariki na kuzikwa Juni 17, 2022 katika makaburi ya kitongoji cha Kasisiwe kilichopo Mkoani Rukwa, na tayari Jeshi la Polisi limekemea vitendo vya kihalifu kwa kusema halita mvumilia mtu yeyote atakayejihusisha na matukio ya uvunjifu wa sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa, ACP Theopita Mallya

Wananchi kupewa ufahamu mipaka ya Vijiji na Hifadhi
Wawili wadakwa kwa kujiuza mtandaoni