Baada ya Mwanariadha wa Tanzania Gabriel Geay kushika nafasi ya pili katika mbio Boston Marathon juzi Jumapili (April 16), wanariadha wakongwe nchini wamesema nidhamu na umakini ni miongoni mwa sababu zilizombeba mwanariadha huyo.
Katika mbio hizo zilizofanyika juzi jijini Boston nchini Marekani, Geay alimaliza nafasi ya pili baada ya kutumia muda wa saa 2:06:04 akitanguliwa na Evans Chebet raia wa Kenya, aliyeshika namba moja baada ya kutumia saa 2:05:54.
Nafasi ya tatu katika mbio hizo ilishikwa na Mkenya Benson Kipruto, ambaye alitumia saa 2:06:06.
Kutokana na kumaliza nafasi hiyo, Geay alizawadiwa dola za Marekani 75,000 ambazo ni zaidi ya sh. milioni 170 za Tanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanariadha wakongwe nchini nyota ameng’ara wamesema huyo katika mbio hizo kwa kuwa alionyesha nidhamu na umakini.
Mwanariadha mkongwe, Selemani Nyambui, amesema kufanya vizuri kwa Geay kumetokana na umakini aliokuwa nao katika mbio hizo na kuwaheshimu washindani wake.
Nyambui amesema ni wakati wa serikali kuwekeza zaidi katika mchezo huo kuhakikisha wanapatikana wanariadha wengi wenye uwezo wa Geay.
“Muda umefika wa kuwekeza kwa vijana, miaka ya baadaye tupate wanariadha wengine kama wakina Geay kwa sababu mchezo huu una muda wake,” amesema.
Juma Ikangaa, amesema Geay ametumia mpangilio mzuri wa kukimbia ndiyo sababu ya kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo.
Mkongwe huyo anaamini ubora wa mwanariadha huyo umetokana na maandalizi aliyoyafanya kabla ya mbio hizo.
“Mimi nimewahi kuwa mshindi wa pili wa mbio za Boston, nafahamu ugumu na njia za kupata ushindi, Geay amefanya kazi kubwa na kupeperusha bendera ya taifa,” amesema Ikangaa.
Hii inakuwa mara ya nne kwa Mtanzania kushika nafasi ya pili katika mbio za Boston Marathon baada ya Juma Ikangaa kufanya hivyo mara tatu mfululizo kuanzia mwaka 1988, 1989 na 1990.
Felix ameungana na Geay Simbu kuiwakilisha Tanzania Katika mashindano ya riadha ya dunia, yanayotarajiwa kufanyika Julai 19 hadi 27, mwaka huu jijini Budapest, Hungary.