Wakulima wa zao la viazi mviringo kijiji cha Lupila wilayani Makete mkoani Njombe wameiomba serikali kujenga masoko ya pamoja ya zao hilo katika kila halmashauri kama ilivyofanyika katika sekta ya madini ili kudhibiti unyonyaji uliokithiri unaofanywa na wafanyabishara kwa wakulima .
Wamesema kuwepo kwa soko la pamoja kutasaidia upangaji wa bei ya pamoja itayokuwa na tija kwa wakulima ambapo inadaiwa kukosekana kwa mfumo mzuri wa biashara ya viazi umesababisha wafanya biashara kufuata wakulima mashambani na kupanga bei wanazotaka wao kwa kisingizio cha umbali na miundombinu ya barabara.
Stelia Sanga, Alfonce Ndelwa na Maltin Msigwa ni baadhi ya wanakikundi cha wanufaika wa mfuko wa kusaidia kaya maskini (TASAF) ambao wanaendesha maisha yao kwa kufanya kilimo hicho, wanasema mwaka huu soko la viazi limeporoka zaidi kutoka elfu 8 hadi kufikia elfu 2 kwa kg 20 na kusababisha hasara kubwa kutokana na kutumia fedha nyingi katika maandalizi ya shamba na mbolea za kupandia na kukuzia.
“Viazi vinanunuliwa kwa bei ya chini sana yaani bei tunayouzia haiwezi kutupatia kipato ili tuweze kununulia mbolea kwasababu hivi viazi vinatumia ghalama sana, tufike sehamu tuwe na vikao vyetu na kwa maana ya kuzungumzia juu ya soko na tuweze kuwa na soko la pamoja maana kwa sasa tunadhulumiwa” amesema Stelia Sanga
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete, Fransis Namaumbo amesema mikakati iliyowekwa na serikali katika kuhakikisha changamoto ya Lumbesa na unyonyaji mwingine unaofanywa na madalali pamoja na wafanyabiashara kwa wazalishaji wa zao hilo, tayari taratibu wa kuanzisha ushirika utakaotumika kama soko la pomoja ili kuwa nguvu ya kuamua bei ya mazao umeanza.
“Tunaendelea na jitihada za kuhimiza ushirika wazalishaji mali katika eneo hilo ili mazao yauzwe kwenye ushirika ama vikundi na kuwa na ghala la mahali pamoja kwa maana ya mkulima kuwa na sauti, upo wakati tunakabiliwa na tatizo la soko lakini halmashauri kwa kushirikiana na mkoa pamoja na SAGCOT kwa lengo la kuhakikisha wakulima wa nyanda za juu kusini katika kilimo hiki wanalima na kuweza kupata soko unasaidia” amesema Namaumbo
Kutokana na kukithiri kwa umasikini katika kijiji cha Lupila ambacho familia nyingi zimebainika kuwa na mzazi mmoja afisa maendeleo kata ya Lupila Veronica Kalimba na Jakrin Mlosso mratibu wa tasaf Makete wanasema, mpango wa kunusuru kaya masikini nchini umeliona tatizo hilo na kupembua watu 71 wenye hali mbaya zaidi kimaisha na kuwawezesha mradi wa viazi wa umwagiliaji ambao umebaili maisha ya kaya nyingi ambazo awali hazikuwa na uwezo wa kusomesha, kujenga na kupata mlo wa uhakika.
“Mradi wa Tasaf ulitupatia fedha za mradi shilingi milioni 71 ambazo zililenga katika kijiji cha Ukange kilimo cha umwagiliaji, wamenufaika sana kupitia kilimo cha viazi na kilimo cha msimu kama mahindi na vitu vidogo vidogo ambavyo wanalima kwa kumwagilia” amesema Jakrin Mlosso
Miradi 39 ya kilimo, barabara, afya na elimu imetekelezwa na tasaf tangu 2015 katika maeneo mbalimbali wilayani Makete ambapo bil 2.6 zimeshatumika.