Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itahakikisha inaondoa changamoto za wakulima katika msimu mpya wa kilimo ikiwemo kusogeza huduma za mbolea ya ruzuku katika maeneo ya Jirani zaidi na wakulima.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbinga akiwa ziarani Mkoani Ruvuma na kudai kuwa eneo hilo ni tegemeo kwa uzalishaji wa chakula nchini, hivyo ameitaka Wizara ya Kilimo kutekeleza kikamilifu suala la upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa kiasi cha kutosha na kwa wakati.
Aidha, amewasihi wananchi wa Mkoa huo kuacha tabia ya kuuza mazao yote pasipo kuweka akiba kwani usalama wa chakula ni vema kuanzia katika ngazi ya kaya ili Taifa liweze kupiga hatua za kimaendeleo.
Dkt. Mpango pia amewataka watanzania kufanya siasa za hoja, ili kuweza kuharakisha maendeleo kwani utumiaji wa lugha zisizo na staha bila kuonesha changamoto kwa hoja hupelekea uvunjifu wa amani.