Walimu saba wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo la utoro kazini.
Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wilaya Igunga, Hamisi Mpume amewataja walimu waliofukuzwa kazi kuwa ni Paul Msabila wa shule ya sekondari Igunga mjini, Mary Evance wa shule ya msingi Bulunde, Kata ya Nyandekwa, Lazaro Cheyo wa shule ya sekondari Nguvumoja, Leonard Chakupewa wa shule ya msingi Kata ya Ziba, Rogasian Pacho wa Shule ya msingi Kata ya Nyandekwa, Sosthenes Chiboko wa Shule ya Sekondari Kata ya Sungwizi na Faustine Obadia Shule ya msingi Kata ya Ziba.
Mpume amesema walimu hao walifikishwa Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Igunga na walikutwa na makosa mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu, utoro kazini kwa muda mrefu pasipo taarifa yoyote kwa mwajiri wao huku baadhi ya walimu ambao hakutajwa majina yao walipewa barua za onyo baada ya kubaini makosa yao si ya kufukuzwa kazi.
Baadhi ya walimu waliofukuzwa kazi walidai adhabu ya kufukuzwa kazini ni kubwa na haiendani na makosa yao hivyo wanakusudia kukata rufaa huku wengine wakifuatilia fedha za kuachishwa kwao ili wakaanze maisha mengine.
Kaimu Mkurugenzi ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Igunga, Ntulila Hadoni amethibitisha kufukuzwa kazi kwa walimu hao.
Hii ni mara ya kwanza kwa tume hiyo kufukuza walimu wengi licha ya wilaya hiyo kuwa na uhaba wa walimu shule za msingi na sekondari.