Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Akson ameagiza kurejeshwa katika nafasi zao Walimu Wakuu waliosimamishwa kuendelea na kazi, baada ya Wanafunzi wa Shule zao kuonekana wakicheza nyimbo zisizo na maadili, endapo Walimu hao hawakuwepo Shuleni na Mamlaka ya Nidhamu kuwachukulia hatua kabla hawajajitetea.
Dkt. Tulia ameyasema hayo hii leo Novemba 6, 2023 Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa ufafanuzi na kuhoji majibu ya Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda kuhusu tukio la kusimamishwa kazi kwa walimu hao baada ya Wanafunzi kucheza muziki wa Bongo fleva unaodaiwa kutokuwa na maadili.
Amesema, “Kama Walimu hawakuwepo Shuleni na Mamlaka ya Nidhamu imechukua hatua kabla, basi iwarudishe kwenye nafasi zao, na kama walikuwepo basi mamlaka iendelee na utarartibu wake, kwa sababu huwezi kuwasimamisha kazi alafu ndio wakate rufaa kujieleza kama hakuwepo hatua hiyo ilitakiwa kufanyika kabla.”
Awali, katika utetezi wa hoja yake Bungeni Prof. Adolf Mkenda alisema Serikali inajukumu la kusimamia maadili, Malezi na kudhibiti aina ya nyimbo zitakazotumika kuchezwa shuleni zinazotangaza Pombe, Sigara na nyinginezo zinazokiuka maadili na kwamba waraka wa mwisho wa Kamishana wa Elimu ulisistiza hata kwenye mabasi yanayosafirisha abiria yanapaswa kuzingatia hilo.
Alipotakiwa kudhibitisha taaarifa kwamba walimu waliosimamishwa walikuwa shuleni wakati tukio la kuchezwa kwa nyimbo hiyo ikiendelea, Mkenda alisema “hilo ni sula la kinidhamu na kama hawakuwepo wana haki ya kukata rufaa kwa Mkurugenzi, ambaye ndiye aliyewaondoa katika nafasi zao.”
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda aliagiza kuvuliwa vyeo kwa Walimu Wakuu wawili wa shule za msingi Wilayani Tunduma Mkoani Mbeya, baada ya kusambaa kwa kipande cha video kikiwaonesha wanafunzi wakicheza wimbo wa msanii Zuchu, uitwao Honey.