Walinda amani wa Tanzania wanaohudumu kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa (UN), nchini Lebanon UNIFIL wametoa msaada wa vifaa kwenye shule ya Al-Hanan yenye mahitaji maalum iliyopo jimbo la Abbasiyeh Kusini mwa nchi ya Lebanon.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNIFIL, vifaa hivyo muhimu vilivyotolewa wiki iliyopita ni pamoja na vitabu vya kusoma, kalamu za kuchorea, madfaftari, viti vya kukalia darasani na vifaa vya michezo.
Akipokea vifaa hivyo mkurugenzi wa shule ya Al-Hanan Mohammed Al Zein, ameshukuru kwa msaada huo akisema, “utaleta tija kwa wanafunzi hao wenye mahitaji maalum lakini pia zira ya siku mbili ya walinda amani hao shuleni hapo na kuzungumza na watoto kumewapa faraja na furaha kubwa.”
UNIFIL inasema walinda amani wake hufanya shughuli za kijamii kama hiyo ya kutoa misaada mara kwa mara ili kuzisaidia jamii wanazozihudumia sio kwa ulinzi tu bali huduma nyingine za msingi katika jamii.
“Walinda amani wana jukumu muhimu la kuimarisha mahusiano na jamii za wenyeji wakati wakiendelea kushughulikia mahitaji yako muhimu.” Imesema UNIFIL.