Idadi ya watu waliofariki kwa mafuriko yaliyotokea wiki iliyopita nchini Libya yakiambatana na kimbunga Daniel, imefikia watu 11,300, huku athari kubwa zikiripotiwa kutokea katika mji wa Derna, baada ya kutoka kwa ripoti mpya iliyochapishwa na Shirika la Hilali Nyekundu la nchini Libya.
Mafuriko hayo, ambayo hayajawahi kutokea, pia yalisababisha watu zaidi ya 10,100 kutoweka ambapo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu – OCHA imesema watu wengine 170 pia walifariki katika maeneo mengine mashariki mwa Libya huku ikidaiwa kuwa idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.
Kimbunga Daniel, kilipiga katika mji wa Derna wenye wakazi 100,000 Septemba 11, 2023 na hali hiyo, ilisababisha kupasuka kwa mabwawa mawili ya maji ya mto na kusababisha mafuriko ya ukubwa wa tsunami. Maji hayo yalisomba kila kitu na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Makumi ya miili hutolewa nje na kuzikwa kila siku.
Awali, Waziri wa Afya wa Utawala wa Mashariki mwa Libya, alitangaza vifo vya watu 3,252 huku Shirika la Afya Duniani – WHO, likisema miili ya watu 3,958 ilipatikana na kutambuliwa na kwamba kulingana na mashuhuda zaidi ya watu 9,000 hawajulikani walipo na wengi wa waathiriwa walikwama chini ya matope au kusombwa hadi katika Bahari ya Mediterania.