Watu 182 wameripotiwa kufa kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika eneo la mashariki ya Kongo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka na tayari Rais wa nchi hiyo, Felix Tshisekedi ametangaza Mei 8, 2023 kuwa siku ya maombolezo.
Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu nchini DRC, wamesema wamepata miili hiyo wengi wakiwa ni wanawake na watoto, katika kijiji cha Bushushu kilichopo mashariki mwa nchi hiyo.
Gavana wa jimbo hilo, Theo Ngwabidje amethibitisha vifo vya watu hao na kusema shughili za uokozi bado zinaendelea na kudai kuwa huenda vifo zaidi vikaripotiwa.
Msemaji wa serikali, Patrick Muyaya, ameeleza kuwa baadhi ya mawaziri watakwenda eneo la tukio kwa ajili ya kupanga shughuli ya utoaji misaada na jinsi ya kusimamia shughuli za kupambana na majanga kama hayo.
Mvua kubwa nchini humo hunyesha hadi mwisho wa mwezi mei na zinakuja wakati nchi jirani ya Rwanda pia ikiomboleza vifo vya watu zaidi ya 130, waliofariki kutokana na mafuriko yaliyokumba eneo lake la magharibi.