Wanafunzi wanne kati ya 19 waliopata ujauzito wakiwa shuleni katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, wanaendelea na masomo yao baada ya kujifungua ikiwa ni utekelezaji wa mwongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Februari 2022 wa kuwaruhusu wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito kurejea shuleni.
Ofisa Elimu wa Sekondari katika Halmashauri ya Moshi, Benedict Sandy, ameeleza kuwa wanafunzi hao walioacha shule mwaka jana na mwaka juzi wamechagua kuendelea na masomo ambapo miongoni mwao, wawili wapo kidato cha tatu na wengine wawili ni wa kidato cha nne wakihudhuria shule za sekondari za Darajani, Mruwia, Cyril Chami na Uparo.
Mwongozo huo, pia unawapa wanafunzi haki ya kumlea mtoto wao kwa miezi ya mwanzo ya maisha yake. Kabla ya kurejea shuleni, mwanafunzi anatakiwa kushiriki kikao kilichoandaliwa na uongozi wa shule, mzazi au mlezi, na kamati au bodi ya shule ili kujadili namna ya kumsaidia mwanafunzi husika huku ukisisitiza Mwanafunzi kurudi shuleni mwanzo wa mwaka wa masomo katika darasa alilokatiza masomo.
Naye Ofisa Elimu wa Sekondari katika Halmashauri ya Moshi, Benedict Sandy amesema wamefanya juhudi kutoa elimu kuhusu mwongozo huo kwa walimu na Viongozi wa shule tangu walipoupokea hapo awali kwa ajili ya utekelezaji.
Wanafunzi hao wanaorejea shuleni, wanaweza kuamua kurudi kwenye shule ile ile au kuchagua shule nyingine kwa kushauriana na wazazi, walezi na wao ambapo mabadiliko ya shule huwezekana kutokana na ombi la Mwanafunzi.