Mahakama nchini Saudi Arabia imeondoa hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya watu watano waliopatikana na hatia ya mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post aliyeuawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki, mwaka 2018.
Waendesha mashitaka wamesema kuwa walipewa hukumu ya miaka 20 jela baada ya familia ya Khashoggi ambaye alikuwa mwandishi wa habari kuamua kuwasamehe.
Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji maarufu wa serikali ya Saudia, aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Ufalme wa Saudia katika mji mkuu wa Uturuki, Instanbul na maafisa wa ujasusi wa Saudi Arabia.
Serikali ya Saudia ilisema kuwa mwandishi huyo wa habari aliuawa katika “operesheni ambayo haikukusudiwa ” na mwaka uliofuatia Saudi Arabia iliwashitaki watu 11 mahakamani kuhusiana na kifo hicho.
Ripoti kutoka gazeti la Asharq Al awasat, linalomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia imeeleza kuwa, familia ya Jamal Khashoggi imesema hukumu iliyotolewa kwa watu waliomuua ni ya haki, na inaweza kuzuia uhalifu mwingine kama huo.