Mitambo ya mabao ndani ya kikosi cha Simba SC imerejea kikosini baada ya kuwa nje kwa muda kutokana na kutokuwa fiti tayari kuwakabili Tanzania Prisons, kesho Alhamisi (Oktoba 05) kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ni Jean Baleke mshambuliaji namba moja ndani ya Simba SC akiwa na mabao matano pamoja na Luis Miquissone kiungo mwenye pasi moja aliyotoa kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.
Baleke alipata maumivu ya mguu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos dakika ya 45 nafasi yake ilichukuliwa na nahodha John Bocco, Luis hakuwepo mazima katika kikosi hicho.
Meneja wa ldara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa wachezaji wao wanaendelea na maandalizi kwa mechi za ushindani.
“Kuhusu Jean Baleke alipata maumivu kwenye mguu kidogo lakini alipewa huduma na kurejea kwenye utimamu hata kwenye mazoezi ya timu yupo.
“Luis Miquissone hakuwepo kabisa kwenye mchezo wetu dhidi ya Power Dynamos kutokana na kutokuwa fiti, lakini kwa sasa anaendelea vizuri yupo tayari kuelekea mchezo wetu ujao dhidi ya Tanzania Prisons.
“Kikosi kimeshawasili Mbeya kwa ajili ya mchezo wetu wa ligi, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.” amesema Ahmed Ally