Wanafunzi 279 wa shule ya sekondari waliotekwa katika shule ya bweni jimbo la Zamfara Kaskazini mwa Nigeria, wameachiliwa na wamesharudi katika vituo vya serikali.
Gavana wa jimbo hilo Dkt. Bello Matawalle ameliambia shirika la habari la AFP hayo na kuongeza kuwa wanafunzi hao ambao wote ni wasichana wote wako salama na afya nzuri.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameelezea furaha yake kwa kuachiliwa kwa wasichana hao siku chache tangu kutekwa, huku akiahidi hatua kali dhidi ya watekaji.
Kundi la wahalifu lililokuwa na silaha liliwateka wasichana 317 wa shule ya sekondari ya Sayansi iliyoko mji wa Jangebe majira ya saa saba usiku wa Ijumaa.