Wanafunzi wa kike wa shule ya bweni katika eneo la Dapchi nchini Nigeria wamepotea kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram, Jumatatu wiki hii.
Taarifa za kupotea kwa wanafunzi hao zimekuja siku chache baada ya Serikali kudai kuwa wanafunzi wote na walimu wa shule hiyo walifanikiwa kutoroka na kwamba wengine walisaidiwa na jeshi la nchi hiyo.
Serikali imelazimika kuomba radhi kwa taarifa hiyo ya awali ikieleza kuwa chanzo cha taarifa hizo kiliaminika lakini hakikuwa na uhakika na hakikutoa taarifa sahihi.
“Tumebaini kuwa chanzo chetu kilichotupatia taarifa hakikuwa cha uhakika japo awali tulikiamini,” imeeleza taarifa hiyo ya Serikali.
Wanaharakati wa kundi la ‘Bring Back Our Girls’ ambalo lilianzishwa miaka minne iliyopita baada ya wanafunzi 276 wa kike wa Chibok kutekwa na Boko Haram, imeitaka Serikali kuweka wazi orodha ya majina ya wanafunzi wa kike ambao wametekwa Jumatatu.
Awali, wazazi walidai kuwa wanafunzi 100 wa kike walipotea kufuatia mashambulizi ya Jumatatu, lakini taarifa ya vyombo vya Serikali imedai kuwa ni wanafunzi takribani 50 na kwamba wengi wao hawajatekwa bali wamejificha porini wakihofia maisha yao.
Shirika la habari la Reuters limewakiriri wazazi na maafisa wa Serikali kuwa wasichana wawili walipoteza maisha, 76 wameokolewa na jeshi; na takribani 13 hawajulikani walipo.