Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa ili zisilete madhara na usugu kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania PST, Mfamasia Fadhili Hezekia alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Semina hii kwa waandishi wa habari tunalenga waweze kutumia taaluma hii ya famasi katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusiana na Afya hasa tabia ya matumizi holela na yasiyo sahihi ya dawa ambayo zinaleta changamoto katika maswala ya kiuchumi nchini,” amesema Mfamasia Hezekia.
Pia, Hezekia ameainisha majukumu ya chama cha wafamasia ikiwa ni pamoja na kutumia weledi, fusra kwa kushiriki kuboresha huduma za upatikanaji wa bidhaa za Afya Tanzania kwa kushirikiana na wadau kutoka nchini mbalimbali.
Katika kudhihirisha hilo amesema wameandaa maonesho ya kwanza yanayoitwa Farmatech East Africa, ambapo bidhaa za Afya za teknolojia za kisasa zitaoneshwa na washiriki zaidi ya 60 watashiriki kutoka Tanzania ma nchi nyingine.
Mfamasia Hezekia amewakaribisha wataalamu, wanafunzi na wananchi katika maonesho hayo yatakayofanyika kuanzia Augusti 30-01 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.