Shirikisho la Wanahabari nchini Kenya, limetoa siku saba kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kutoa taarifa juu ya hatua ilizochukua za kuwafungulia mashtaka Polisi na watu waliohusika kuwashambulia na kuwapora vifaa vya kazi Waandishi waliokuwa wakiripoti maandamano yaliyoitishwa na upinzani.
Hatua hiyo, imetolewa ikiwa ni muda mfupi tangu Wanasiasa wa mrengo wa Chama Tawala kutoa matamshi yaliyotafsiriwa kama kitisho kwa uhuru wa vyombo vya habari huku Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Erick Oduor akisema ujumbe wao unalenga kujua hatma hiyo na si vingine.
Kupitia hotuba iliyotolewa kwa Taifa na Rais wa Kenya, William Ruto kuhusu uhuru wa wanahabari amesema Serikali haiungi mkono vitendo vyovyote vinavyotishia Wanahabari huku akisisitiza imani yake juu ya uhuru wa vyombo vya habari na hivyo haungi mkono kitendo chochote kinachomuweka Mwanahabari katika mazingira hatarishi.
Wanahabari hao, walijeruhiwa na vifa vyao vya kazi kuharibiwa na waandamanaji pamoja na Maofisa wa Polisi pindi wakati walipokuwa wakiwajibika kuripoti maadamano ya upinzani nchini humo, yaliyoitishwa na kinara wa upinzani nchini humo, Raila Odinga ambayo tayari yamesitishwa ili kutoa nafasi ya kufanya majadiliano.