Waandishi wa habari nchini wamehimizwa kuzifahamu sheria za habari ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa marekebisho ya sheria hizo unaoendelea.
Hayo yamebainishwa katika mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN), kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Vyombo vya Habari (IMS), na mwezeshaji Jesse Kwayu katika msisitizo wa mada zilizotolewa kuhusu sheria za habari kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Mtwara.
Amesema, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanahabari mkoani humo, ikiwemo kuvifahamu vipengele vya sheria vinavyokandamiza uhuru wa habari, na upatikanaji wa taarifa ili waweze kutoa maoni ya kuboresha sheria hizo.
Awali, akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Habari na Utafiti wa MISA TAN, Jacquiline Jones amesema umuhimu wa mafunzo hayo, unatokana na ukweli kwamba waandishi wa habari ndio wanufaika na wahanga wa sheria hizo.
“Wanahabari ndio wanaozitumia sheria hizi hivyo ni muhimu kuzijua. Hivyo, mafunzo haya ni mahususi katika kuwaongezea uelewa sahihi utakaowasaidia kuzitumia na kubaini changamoto zilizomo na kupendekeza marekebisho yake,” amesema Jones.
Washiriki hao, wamejifunza vipengele mbalimbali vya sheria zikiwemo Sheria ya Huduma za vyombo vya Habari ya 2016, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya Mwaka 2016, Sheria ya EPOCA, na Sheria ya Uhalifu wa Mitandaoni ya 2015.
Katika mafunzo hayo, washiriki hao 36 walibadilishana uzoefu utokanao na utekelezaji wa sheria hizo, na kuishukuru MISA TAN na IMS kwa kuwapatia elimu na kuahidi kuitumia katika kuboresha utendaji kazi na chachu ya ushiriki wa mchakato, wa marekebisho ya sheria za Habari nchini.