Wananchi wa Kata ya Rutende wilayani Uyui mkoa wa Tabora wamefunga ofisi za serikali ya kata hiyo wakipinga uongozi uliopo kwa madai kwamba hauwasaidii.
Tukio hilo limetokea leo tarehe 12 Aprili 2019 ambapo wananchi hao waliifunga ofisi wakishinikiza uongozi uliopo uondolewe na wachaguliwe viongozi wengine.
Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gifti Msuya alilazimika kwenda kuzungumza na wananchi hao katika ofisi za Serikali ya Rutende zilizoko katika Kijiji cha Itaga ili kusuluhisha mgogoro huo.
Wakati akizungumza na wananchi hao, Msuya aliwataka watendaji wa kata hiyo kuwajibika kwa wananchi ili kuepuka migogoro isiyo na lazima.
Aidha, Msuya amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia hatua mkononi badala yake wafuate vyombo husika vya maamuzi.