Klabu ya Liverpool imethibitisha kuachana na wachezaji wake wanne mwisho wa msimu huu; James Milner, Roberto Firmino, Naby Keita na Alex Ox-lade-Chamberlain.
Wachezaji hao ambao wote walikuwepo kwenye kikosi cha Liverpool kilichotwaa Ubingwa wa Ulaya mwaka 2019 na Ubingwa Ligi Kuu England msimu uliofuata wanaondoka wakati mikataba yao ikiwa inaelekea ukingoni.
“Wachezaji wetu wanne wataondoka na shukrani zetu kwao kwa mchango wao ambao wameutoa kwetu,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Liverpool.
Klabu hiyo imeongeza kuwa itawapa heshima maalumu wachezaji hao kwenye mechi yao ya mwisho ya nyumbani ya Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa, kesho Jumamosi.
Milner na Firmino walijiunga na klabu hiyo mwaka 2015 chini I ya Brendan Rodgers na waliandika historia ya kutwaa ubingwa England mwaka 2020, ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho miaka 30 iliyopita.
Imeelezwa kuwa Brighton wanakaribia kumnasa Milner mwenye umri wa miaka 37 ambaye ameshinda mataji sita akiwa na Liverpool huku akiweka historia ya mchezaji wa tatu kucheza mechi nyingi za ligi hiyo, 617.
Firmino, 31 ambaye ni mfungaji bora wa Brazil wa muda wote katika Ligi Kuu England akiwa amefunga mabao 80 katika mechi 254, lakini akiwa hajatumika kwenye kikosi cha Liverpool tangu mwezi Machi, mwaka huu.
Mbali na hilo, Firmino maarufu Si Senor atakumbukwa zaidi Liverpool katika kipindi chake alipokuwa akicheza sambamba na Mohamed Salah na Sadio Mane kama sehemu ya wachezaji watatu mahiri washambuliaji chini ya Jurgen Klopp.
Klopp alieleza kuwa alitamani Firmino aendelee kusalia huku kukiwa na maongezi juu ya hilo lakini mwenyewe amechagua kuondoka.
Upande wa Keita aliyefunga mabao 11 katika mechi 129, alimwaga saini ya kujiunga na klabu hiyo mwaka 2017 lakini msimu huu amecheza mechi 12 pekee kutokana na kusumbu- liwa na majeraha.
Wakati huohuo, Oxlade-Chamberlain amekuwa akipambana kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza msimu huu akiwa amecheza mechi 13, ya mwisho ikiwa waliyopoteza dhidi ya Real Madrid kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, alijiunga Liverpool mwaka 2017 akiwa amecheza mechi 146 na kufunga mabao 18 tu.
Hata hivyo, Liverpool ambayo haikuwa na msimu mzuri msimu huu, inalazimika kuingia sokoni kufanya usajili wa wachezaji wapya ikiwa tayari imemsajili kwenye dirisha dogo, Coady Gakpo kama mbadala wa Firmino.
Lakini pia Majogoo hao wanatajwa kuiwinda saini ya kiungo wa Chelsea, Mason Mount na Muargentina aliyekuwa kwenye kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia 2022 anayekipiga Brighton, Alexis Mac Allister kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao.