Baada ya kufanikiwa kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza, Klabu ya Young Africans imepongezwa na kupewa mbinu za kucheza hatua hiyo ili kufanikiwa kutwaa Ubingwa dhidi ya Klabu kutoka Afrika Kaskazini.

Young Africans itacheza Fainali ya michuano hiyo dhidi ya USM Alger ya Algeria ambao wao waliitoa Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0. Fainali ya kwanza ya michuano hiyo imepangwa kupigwa Mei 28, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Juni 3, nchini Algeria.

Pongezi na siri za kutoboa kwenye mchezo wa Fainali, zimetolewa na Kocha Msaidizi wa AS Vita ya DR Congo, Raoul Shungu ambapo ameionya klabu hiyo ya Dar es salaam kuwaambia kama wanataka kombe hilo basi wahakikishe wanajitoa kwa uwezo wao wote.

Shungu ametoa kauli hiyo kufuatia Young Africans kufuzu fainali ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1.

Shungu amesema kuwa Young Africans wana kila sababu ya kujipongeza kwa kuweza kufikia hatua hiyo lakini wanapaswa kutambua kazi kubwa iliyopo mbele yao ni wachezaji wa timu hiyo kuweza kujitoa zaidi ili kufikia malengo ya kuchukua ubingwa huo.

“Binafsi kwanza niwapongeze Young Africans kwa hatua kubwa ilipiga kwa kuweza kufika fainali ya Kombe la Shirikisho kwa sababu ni jambo kubwa na imekuwa ni mara ya kwanza upande wao kuweza kufikia hatua hiyo lakini ukiangalia kwa sasa tayari wa ubingwa wa Ligi Kuu tayari na sasa wanaenda kucheza fainali ya Afrika kitu ambacho ni kikubwa kwa kuwa wachezaji wao wamejitoa kwa nafasi kubwa.

“Lakini wanatakiwa kujua kazi iliyokuwa mbele ni kubwa na ngumu zaidi kwa sababu fainali kila timu huwa inakuja na mpango ambao huenda hakuwa umeutarajia na ninachotaka kuwaambia wachezaji wanatakiwa kujua ukubwa wa jukumu la mechi mbili za fainali ya CAF ambayo wanatakiwa kuipigania kwa kujitoa zaidi pamoja na kuongeza nidhamu ya mchezo kutokana na aina ya timu wanayokwenda kucheza nao,” amesema Shungu

Wanaopewa mkono wa kwaheri Liverpool watajwa
Ugonjwa wa figo wakumba asilimia 7 ya Watanzania