Wakati mashabiki na wadau wa soka wakicharuka kwa kulitaka Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’, kumtaja mchezaji wa Young Africans aliyesababisha Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’, kuifungia klabu hiyo kusajili kutokana na kukiuka kanuni ya uhamisho, mchezaji ambaye amekuwa akidaiwa ndiye mhusika wa kifungo hicho mitandaoni, Pacome Zouzoua, ameibuka na kutoa neon.

Aprili 12, mwaka huu, TFF ilitoa taarifa kwa umma kuwa FIFA imeifungia Young Africans kusajili kutokana na kukiuka kanuni ya uhamisho za kile kilichoitwa Annexe 3 ya Kanuni ya Uhamisho (RSTP) ya shirikisho hilo.

Ikasema Young Africans haikuingiza uthibitisho wa malipo wa uhamisho wa mchezaji husika (ambaye haikumtaja) katika usajili (TMS), licha ya kukumbushwa kufanya hivyo, jambo ambalo wadau wa soka nchini wamekuwa wakiipigia kelele TFF kupitia mitandao ya kijamii wakiitaka kumtaja mchezaji huyo kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa wengine.

Lakini pia kupitia mitandao ya kijamii, wadau mbalimbali wa soka wameenda mbali wakidai mchezaji huyo ni Pacome na kwamba Young Africans imekuwa ikitumia kivuli cha kuwa majeruhi tangu alipoumia mechi dhidi ya Azam FC, ndiyo maana haimchezeshi ikihofia kupokwa pointi nyingi endapo Sekretarieti ya Nidhani ya FIFA ambayo suala hilo lipo mezani kwao kwa ajili ya hatua zaidi, itakuja na maamuzi kama hayo.

Aidha, walifafanua zaidi kuwa endapo kama kweli alikuwa majeruhi, timu yake ya Taifa, Ivory Coast isingemwanzishia benchi katika mechi mbili zilizopita za kirafiki zilizopo kwenye Kalenda ya FIFA.

Hata hivyo, Pacome ameibuka na kusema yupo fiti kwa asilimia 100 na kwamba amemuomba Kocha Miguel Gamondi dakika 10 hadi 15 za kumpanga katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRBD Bank dhidi ya Tabora United kesho Jumatano (Mei Mosi).

Akizungumza jijini Dar es salaam, amesema mara kwa mara alikuwa akifanya programu maalum za mazoezi anazopewa na kocha wake wa viungo na pia anaendelea na tiba alizopewa na kufanya mazoezi ya Gym ya majuma kadhaa na programu zingine za kuweka mwili sawa.

Amesema anajihisi vibaya kuona wachezaji wenzake wanapambana na kupigania timu huku jina lake halipo kwenye karatasi ya kikosi cha timu ambacho kinaingia katika vita vya kusaka pointi tatu za mashindano mbalimbali wanayoshiriki.

“Binafsi niko sawa nikipata nafasi ya hata dakika 10 au 15 naamini nitarajea na kuwa sawa na kuendelea kushirikiana na wachezaji wenzangu kwenye kufanikisha kusaka ushindi kwa kila mechi kufikia malengo yetu ya kutetea mataji ikiwamo michuano ya shirikisho na ubingwa wa Ligi Kuu,” amesema Pacome.

Ameongeza kuwa wanatakiwa kuchukuwa ubingwa kwa kuwa ni malengo yao, anajua ugumu upo lakini wanajaribu kufanya wanachokiweza ili wafanye vizuri na kufikia malengo yao na kuendelea kuwapa furaha mashabiki wao.

Kuhusu tofauti ya soka la Tanzania na Ivory Coast. Pacome amesema Tanzania kuna mashabiki wa kweli na wenye mapenzi na timu zao tofauti na taifa lake, ambapo hakuna wanaojitokeza uwanjani kusapoti.

“Tanzania wanakuja uwanjani kusapoti timu zao, kitu ambacho nakipenda sana, lakini nyumbani si rahisi kwa mashabiki kuja uwanjani kutazama mechi, uwapo wa mashabiki unaipa thamani ligi ya Tanzania.”

“Pia mashabiki wanaongeza kitu kwa mchezaji, nimeenda Uwanjani kutazama mechi mara mbili kipindi nikiwa majeruhi, watu wananiita na kuniombea nipone haraka na kunipa motisha, hii inanipa nguvu na kuona nina maana kubwa sana kwa hawa watu na kutakiwa kufanya kitu kitakachowapa furaha nitakaporejea uwanjani,” amesema Pacome.

FC Barcelona inajitafuta kwa Guido Rodriguez
Mgunda kuanza Simba SC bila wachezaji sita